Monday, November 29, 2010

Wivu wa chuki!

Jazba hainisaidii duniani. Wivu wa chuki ni aghali maishani. Nikahitaji nini kushiriki na huyu katika kufanikisha maisha huru ya watu wengi? Nijikombe vipi kwa ng’ombe anipaye kwato ninyonye damu? Nitaruka vipi na mbayuwayu wenzangu hili khali nimenyonyolewa mbawa na manyoya yote lowana? Dunia haiishi maajabu. Maisha ni changamoto, changamoto ngumu na zenye kubadilika kila sekunde. Maisha ni mchezo wa mapambano, cheza vizuri, cheza sana kwa bidii yako yote lakini tambua leo utashinda kesho utashindwa. Usikate tamaa na wala usijitenge na timu yako nzuri yenye ubunifu ukadhani kwamba kuna timu ishindayo siku zote, hakuna.

Adui wapo na rafiki pia. Nani rafiki yako mkuu? Mtu fikirika matendo yangu ni fumbo, rafiki yangu mkuu ni mimi mwenyewe. Kushiriki au kutoshiriki kitu na yule au wale si kitu katika kukamilisha karama na kalamu yangu. Kama hawa hawataki kuwa nami basi wale watakuwa nami na ni wazi siwezi ishi pasipo wewe au wao, adui au rafiki. Nikiwa peke natembea nafurahi sana kwani mimi katika mimi ni kiumbe kamilifu. Nikiwa nanyi sintokuwa mjuaji katika ninyi kwani mimi katika ninyi nina mapungufu mengi.

Umoja ujenga imara ya kitu na utengano udhoofisha juhudi ya jumuia ya watu na kuleta kitu dhaifu. Umoja wangu na wanyonyaji hauna tija zaidi ya kunyonya wengine zaidi na kunyonywa mie nikadhoofu. Umoja wangu na wanye haki ni heri na fanaka ya maisha yangu na wengine wengi. Kwa hilo sintoenda katika shauri la wasio haki. Nitashiriki vipi na rafiki niishie nae chumba kimoja ili hali ana kula pamoja na wasio haki? Mie mtu wa haki, naogopa shiriki na yule hasiye haki kwani wengi huwa na jazba katika kuongelea haki na kushikiria imani isiyo nyonyaji.

Friday, November 26, 2010

NIMECHAFUKA….

Kovu likune kwa tahadhari. Nikawe wa ajabu vipi kukuna kovu kwa kutumia tupa? Nini nataraji kiumbe mie katika kovu hilo? Ndio kidonda kilinitesa na kunikosesha raha, kiliniletea hasira wakati mwingine, kilivunda na kunuka, kiliwaita nzi karibu nami, ila kimepona na leo naonesha jeuri ya kukuna kovu lake kwa kutumia tupa. Kwa kidonda hiki naweza sema nilikula ndizi na maganda nikaokota mwenyewe. Nakumbuka na kusahau mateso ya kidonda hiki. Sijui nimetoa wapi jeuri ya kukuna kovu hili tena kwa kutumia chuma.
Nilijiamini mimi ndiye kiumbe mwenye afya na nguvu ya upinzani mwilini, mwili wangu nadhalia haukuingia gonjwa na wala uchafu, nilikuwa safi nilo safishwa na kusafishika. Kila damu na radha yake, si wote watamanio kuniona mie msafi na ndivyo hivyo nilipata donda, lilinikasirisha nikakasirika. Ni pigo nilolipata toka kwa kundi la watu wachafu, watu walio adui wa afya yangu ya akili na mwili, mie ni mpinzani wa kweli kwao, walinitambua kuwa kila unywele kichwani mwangu umejaa upinzani kwa kila watendalo watendalo. Niliwafumbia macho na kuwazibia pua ili nisione uchafu wao na wala nusa harufu mbaya toka kwao, nilijidhatiti kwa yote ili nibaki msafi takasika.

Naishangaa nafsi yangu kwamba nakula sahani moja na hawa wachafu leo. Natumia kijiko kimoja nao bila kuambia kimeoshwa kwa maji gani. Twaletewa mbege katika kikale na mie natumbukiza mrija wangu kunyonya utamu pasi kuwa na wazo la usafi ndani yangu. Je! Nini kimenisibu na kupofushwa na watu hawa? Makovu ya watu wangu nayakuna kwa tupa katika kundi la watu hawa wachafu wa nafsi na miili. Vidonda vya watu wangu vikirudi nani atavipatia pulizo vitulie?

Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Ilo safi haina umoja na ilo chafu. Na kama umoja huo utakuwepo basi safi nayo itakuwa chafu. Nimechafuka pasi kujitambua.

afrotanza gallery