Nilijitazama nikafurahia ngozi yangu. Ngozi nzuri nilo pewa na Muumba. Inang’aa iso na kovu. Wote walitambua hilo pindi walipo niona ingawa walijua fika mie mtu shamba. Mtu shamba nilo pewa lift ya kuingia mjini.
Hapo nilipo wekwa ndo panishangaza. Akili yangu yashindwa tofautisha ungo na mwamvuli. Mvua yanyesha na nimejifunika ungo kujikinga. Ninalowa hili hali nimejifunika.
Nimezungukwa na watu wengi. Tunaangaliana tunafurahi. Wengine kati yetu wananuka na wanafuatwa na nzi. Hawajifichi lakini hakuna hata mtu mmoja anayediriki waambia wakae mbali nasi wajioshe watakasike. Ninasikia tetesi kwamba wao ndo wameshika fungua ya basi tutumialo kwa safari. Ni maneno chinini tu kwamba kuna harufu mbaya lakini hakuna anyoshaye mkono kwa hawa jamaa zetu walio jaliwa na nzi. Mmmh! Nisitie chokochoko mtu shamba mie nikarudishwa polini.
Donda halifugwi mtu shamba nasema wazi. La mwiba au la jembe donda litibie. Tunawakalia kimya hawa watu watazidi tunyambia na kutuchafulia hewa. Tunawaona na kuwajua lakini kuwasema na kuwatenga nasi ili wajiweke swafi twaona haya. Donda lionee haya na usilitibie litakuumbua. Litavunda na kutoa harufu mbaya. Harufu hiso furahisha, harufu ino kera na mwishowe kiungo beba donda kitaoza. Ogopa mana lakuvunda halina ubani.
Mie mtu shamba nimefundishwa haya, siwezi inua mkono kuwaonyesha kidole changu kwa yeyote mchafu mana kwa kufanya hivyo ntarudishwa polini. Mie mtekelezaji na wala sio muamuzi. Hata kama nikimuona yule kati yetu ameshika kinyesi sintoweza mwambia chochote nitamchekea tu ingawa mie pia nakereka na harufu ya kinyesi chake.
Donda halifugwi, Chambuka Chanika Maimuna, donda halifugwi!
No comments:
Post a Comment