Monday, April 12, 2010

MIMI NA WEWE WOTE WEHU!

MIMI NA WEWE WOTE WEHU!

Pole mwehu mwenzangu kwa uvumilivu ndani ya basi letu, basi lililo na viti tusiweze vikalia, basi lililo na vioo tusiweze vifunga, basi lililo na taa tusiweze ziwasha, basi lililo na saa pia tusiweze tambua muda.

Pole kwani faida tuipatayo ni kusimama safari yetu yote mpaka kituo hiki, kituo cha kuchagua dereva na kondakta mwingine, hatukuweza funga vioo na matokeo yake vumbi, jua, na mvua vimekuwa vyetu safari nzima, usiku mchana pia tumekuwa buruzwa kwani hawakuweza washa taa za basi letu kuona wapi tulipo na wapi twaelekea, safari yetu imekuwa ngumu kwani hatukutambua majira ya siku, wiki, mwezi na hata mwaka.

Ninafuraha kuu kwani sisi hutuna tabia ya kulalamika, sisi ni wapole tusiopenda kelele na tumekuwa wanyoofu kwa kuinama chini kama kondoo.

Tulipo ianza safari yetu walituhadi mengi, mengi kweli walitutamkia. Hawakuwa na woga wowote, walituambia watatuwezesha tuweze kaa na kustarehe ndani ya basi letu, watafunga vioo na kuwasha AC ili tusinzie kama tuko peponi, kwamba watawasha taa pindi tutakapo taka ona ili sisi pia tuelewe muelekeo wa basi letu, watawasha taa ili tuweze ona pindi kiza kitapo wadia, kwamba saa itaheshimiwa kwani watatusomea na kuzingatia muda kadri ya matakwa yetu na walituahidi kulilinda basi letu kwa wavamizi na wezi wa ndani na nje pia .

Pole kwamba tumefika hapa wao mwenyewe hawatambui kwanini wameshindwa kamilisha yale walio tuahidi, maisha bora kwa kila abiria na hawaelewi kwa nini basi letu ni bovu. Wanajua na ukondoo na aibu zetu tunawaangalia kwa jicho la chinichini, tunashindwa tamka kwani tabasamu zao ni mvuto sana kwa wengi wa wehu wenzetu. Wanatambua wameshindwa kutuweka bora tukae tutulie tufaidi safari yetu na kukuacha tuteseke, tutoke jasho na tunuke ujinga.

Sisi ni watu wazuri sana, hata tukichomwa sindano hatushituki, tumeridhika na hali duni ya basi letu, tumeridhia vifaa vya basi letu chukuliwa na wapita njia, buzwagi nyamongo pia sisi hatujalalama, tumeipenda staili ya sisi potezwa njia na kuingia njia zilizo tugharimu pesa nyingi kama njia za rites na tics.

Sisi kweli ni wavumilivu, twapaswa jisifu. Ingawa wao na wahudumu wao wengi wanatope, wamechafuka. Wamechafuka kwa kushikana mikono na wale wachafu au kushiriki kuogelea kwenye tope. Tunawavumilia kukaa nao ingawa wananuka uvundo, hatujawachoka kama ilivyo kawaida yetu.

Wanatambua kuwa wanakashfa mbali mbali, sisi tumenyamaa na kuwapa sifa na kuwapigia makofi kwa mwendo mbaya na kutuburuza vyema. Wao kweli wanatuunga mkono kwani kashfa zao kwetu sifa. Wanatambua kati yao kuna mafisadi, wanachekelea na sisi na wehu wetu tumewaunga mkono katika kicheko hicho na kuwaacha waendelee kufaidi na kutunyonya vilivyo. Wanatupa pongezi nyingi, hatuna wivu na tuna uvivu kichwani. Masikio tumeweka pamba, wanao wasema waseme na usiku watalala na sisi endelea buruzwa na basi bovu kama lilivyo.

Imeongelewa BOT kuna wizi, tumewafurahisha kwa ukimya wetu katika hilo. Inapendeza kwani tuna busara na tunatambua kuwa BOT hela haziishi. Hata kama zitaibwa saba mara sabini. Ikaja Richmond na sera zake za unyonyaji na udanganyifu, hayo wamepiga zile tiktaka na kutupiga bao, hatukuelewa hata mpira umetupitaje, wametupiga bao na kutufumba midomo, sisi pia tumefumba pasi na shaka, tena tumeridhia ujanja ujanja wao.

Wamenunu rada ili wawe na uwezo wa kuzuia kunguru wasinyee basi letu, tena bila sisi wenye basi toa maoni yetu na vipaumbele katika safari yetu, ikatambulika kuna rushwa katika hilo. Walicheka wakigonga glasi zao, tena sana kwani tuliwafurahia na kuwashangaa waongeleao rushwa, hata kama kuna rushwa kwani sisi wehu tumepungukiwa nini? Hii ndio rangi ya basi letu, halijachafuka na sisi tumesha izoea rangi hii.

Wehu wenzetu wakapanua midomo kupayuka hovyo kuwa, kuna abiria wameamishwa sehemu zao kumpisha mzungu. Wao wakatabasamu na kutamka yaani uache mtu mweusi atambe wakati mzungu kaja? Wakaendelea tukebehi kuwa lini tutajifunza kizungu kama hatuta kubali wehu na wachovu wenzetu waache sehemu zao na kuwaachia wazungu nafasi nzuri na kubwa za kutosha? Mzungu nae katia sumu mtoni ambapo wehu wenzetu huko Musoma unywa maji yake na utumia kwa shughuli mbalimbali kwani maji ni uhai. Sisi kweli ni wema kwani hayo tumeyafumbia macho.

Hawa wehu wenzetu wanawachekesha sana, eti mtu kushika chaki anawapigia kelele, anawakondesha, yaani kwao ni maajabu sana. Waache kwenda ulaya kusaini uuzaji wa vifaa vya basi letu wawawezeshe wehu washika chaki? Waache kula kuku kwa mrija na kugonga glasi za mvinyo wamjengee mshika chaki nyumba nzuri ya kuishi? Wametufunga midomo tukafie mbali, kushika chaki tunataka hali nzuri ya nini? Nani tunamfaidisha? Kwanza waonavyo ni bora tusipewe chaki bali mkaa ili wapate vinono na kwenda kujenga mahekalu ya kuvutia na ya kupendeza ili wao na familia zao waishi maisha ya peponi, wehu tukizidi taabika.

Wamekaa kimya wakiwangalia wehu wenzetu, wehu wanaojiita wafanyakazi, kwamba nao wanajisumbua kupanga mgomo, wanatusihi tuwasemeshe, hawajui watendalo. Sisi kweli tumekaa kimya wehu wenzetu wapambane kivyao vyao mana kila mtu atauchukuwa mzigo wake. Wehu wenzangu, siku ya siku tutakuwa mashahidi. Wehu wenzetu wataburuzwa na virungu na kukiona cha mtema kuni kana kwamba ni wavamizi ndani ya basi letu.

Mwehu mwenzangu. Tulio wapa udereva na ukonda wamekaa juu ya basi letu wakila vyuku na bia, wanatucheka jinsi walivyo tuburuza Mwanzo wa msimu mpaka hapa tulipo. Wanajiandaa omba nafasi ya kutuongoza na kuliendesha basi letu kwa mara nyingine. Wanajisifu kwamba kwa kanga, kofia, t-sheti na wali tutawachagua tu. Mie najua ni wehu tulionao ndio utatupelekea tuwape nafasi nyingine ya kutuburuza na kutuacha taabani na basi letu. Wanatuambia tusichoke, tuwachague tena sisi wehu ili tuendelee kula msoto, ukondoo wetu ndio chanzo cha wao kutuburuza.

Wanatusihi tusikose siku ya kuchagua, ewe mwehu mwenzangu uwahi mapema kufika kituoni na umchague bila shaka mwizi na dereva asiye na utambuzi wa nini cha kukufanyia ili kukuokoa katika mchoko na uchovu ulio nao na akuburuze kwa hali ileile na kasi ileile.


No comments:

afrotanza gallery