Thursday, April 22, 2010

NITAKUWA KIPOFU MPAKA LINI?

Kweli kipofu hawezi mwongoza kipofu. Hata ningekuwa wa hali ipi siwezi lenga kile nisicho kiona na nikifanya hivyo nitakuwa sitambui kama ni nini nimekifanya na kwa manufaa gani.

Jongoo hakujaliwa vaa saa lakini ana busara sana ya kutambua muda na kuutunza. Mimi sielewi majira ya maisha yangu, sijui ni wakati gani niwike na wakati gani nitulie, wakati gani nitafute na wakati gani nile na kupumzika.

Mimi mwanadamu nimekosa nini na wala nisifanikiwe katika maisha yangu? Je! Mungu anaupendeleo? Iweje wengine wafanikiwe mimi niishi kwa manung'uniko?

Yamkini ipo sababu. Tunaambiwa tuwaangalie ndege wa angani hawalimi na wala hawavuni lakini wanaishi. Niwe wa aje niishi maisha ya viumbe visivyo na utashi?

Basi kama hivi ndivyo, mimi kiumbe mwenye utashi sijitambui. Kiumbe nisiye jitambua siwezi fanya kitu chochote chenye manufaa kwangu na kwa jamii yangu. Kuto kujitambua kunanifanya niwe mtumwa, nitegemee mawazo ya watu wengine, nisiwe na maamuzi imara juu ya fikra zangu, nisijue majira ya mwaka wa maisha yangu na wala nisiwe na mvuto kwa maendeleo yangu kihali na kiakili.

Kuto kujitambua kunanifanya niwe muoga, nisijiamini na wala nisiaminiwe, nijawe wivu mkuu na kuwa mtu akili raruka.

Kuto kujitambua kunanifanya niishi maisha ya kusadikika na kuto eleweka. Nisitambue wakati gani napanda na wakati gani nashuka, wakati gani nikimbie na wakati gani nisimame.

Kweli kutokujitambua kunanifanya niwe kama maji. Kwamba umbile langu lategemea birika lililo nibeba. Niwe mtu wa kukimbia tu na nisitembee hata siku moja!

Ndio vidole havilingani, nami nisingependa vilingane. Mungu aliumba usiku na mchana kwa maneno, usiku na mchana viwe. Ikawa usiku na ikawa mchana. Nini maana ya maneno haya kwangu?

Mimi sikujaliwa karama? Mimi sikujaliwa busara? Mimi sikujaliwa maono? Mimi sikujaliwa uchaji?
Mimi sikujaliwa akili?

Kama Mungu aliya niumba alinijalia hivyo na kunipa miti na matunda ya kula iweje niwe masikini? Nitaishi na umasikini mpaka kifo changu? Utungu wa namna gani huu? Au huu ni msalaba wangu niwaokoe watu wa ulimwengu fulani nisio ujua? Yesu aliubeba msalaba kuokoa watu wa dunia hii, mimi ninabeba msalaba huu wa umasikini kumuokoa nani?

Ni kipofu. Nasema tena mimi ni kipofu. Natamani nione na niishi maisha ya mvuto katika nafsi yangu. Natamani nitoke gizani na iwe mchana kwangu, natamani nijitambue na nitambue majira ya maisha yangu.

Machozi yananitoka, nitakuwa kipofu mpaka lini?

1 comment:

Anonymous said...

Good!

afrotanza gallery