Friday, April 15, 2011

KATIBA

Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu akamuumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kitambaacho juu ya nchi.


Kwa waamini kwamba wameumbwa na Mungu, mungu hakumpa mwanadamu mamlaka ya kutawala mwadamu mwenzake. Katika kundi kubwa la watu au wanyama hatuwezi wote kuwa mbele, ni lazima wachache kati yetu tuwatangulize kama wawakilishi wetu kwa kufuata taratibu tulizo ziweka sisi wenyewe wana kundi au wana jamii fulani. Taratibu ambazo kila mwanajumuia ameridhika nazo na hana shaka ni kwa manufaa ya kila mwanajumuia. Taratibu hizo zitaridhiwa na wote wanaotaka kutuongoza ili tufikie pale ambapo wote tumetazamia kufika bila kuwa na manung'uniko yoyote kwa wale wa mbele na wale wa nyuma.


Kuweka taratibu ambazo zitaridhiwa na kila mwana jumuia ni kazi ngumu na inahitaji utulivu mkuu. Kila kiumbe anamaono tofauti, kila kiumbe ana nafsi ya kipekee, makubaliano ya viumbe wenye hulka tofauti yanahitaji utulivu wa mkubwa na mdogo, mwanamke na mwanaume, vijana na wazee. Mchanganyiko wa wanawake na wanaume, vijana na wazee unaweza kuwa ndio mchanganyiko utakao leta manufaa ya makubaliano ya taratibu za kuendesha jumuia husika. Pasiwepo mjuaji wala tamaa ya kitu fulani katika kuandaa kitu cha manufaa ya jumuia kwa muda mfupi au mrefu.


Kulinda na kuenenda kutokana nataratibu ambazo jamii fulani imeziweka ni jambo la lazima katika jamii hiyo. Mtu aliye yote anapo kiuka taratibu hizo ataadhibiwa kutokana na taratibu hizohizo ambazo jamii imeziweka kwa maslahi yao wote.


Taratibu za maridhiano ya viongozi na waongozwa uitwa KATIBA. Si kazi rahisi kuandaa katiba mpya itakayo ridhiwa na watu zaidi ya milioni 40 kiurahisi. Katika kuandaa katiba kila mwanajumuia anatakiwa kushiriki vyema maana katiba ni mali ya watu wote wa jumuia fulani. Jumuia inayofanikiwa kuandaa katiba iliyoridhiwa na watu wengi katika jumuia hiyo ni jumuia yenye mafanikio, ni jumuia ya upendo, ni jumuia mtu kwa watu na watu kwa mtu kwani ni kwa ajili ya manufaa ya wote. Kazi ya uandaaji wa taratibu za kuendesha jumuia ya watu zaidi ya milioni 40 yahitaji muda na busara kuu.


Kutoa muda wa siku nne kuchangia maoni ya muswada wa katiba mpy ya jamuhuri ya muungano ni kichekesho. Watawala nao yaelekea hawajui nini maana ya katiba. Pupa pupa ifanye kwenye maisha mengine na si katika kuandaa katiba. Katiba haitungwi kwa ajili ya watu waishio mijini pekee, hapana, katiba ni ya watu wote wa mijini na vijijini. Tumesikia sehemu zilizo tumika kupojea maoni juu ya muswada wa katiba mpya, katiba kwa ajili ya Jamuhuri ya muungano wa tanzania. Ni mijini, hakuna watu wa kuchangia chochote waishio vijijini, hii ni hatari. Katika katiba hakuna masikini na mkokoteni wake au tajiri na gari lake. Katiba mali ya wote, hivyo kila mwanajumuia, mjini au kijijini, msikitini au kanisani anatakiwa kushiriki vyema katika uandaaji wa katiba.


Watanzania washikamane wawe imara katika kuhakikisha yale yote ambayo yameonekana ni mapungufu ya jumuia yetu kutokatana na katiba iliyopo yanaondoka na kupata katiba mpya na safi kwa manufaa ya mla mkate hotelini na mla muhogo shambani. Kuhakikisha katiba inakuwa wazi katika uwajibikaji wa kila mtanzania, katiba isiruhusu kuwepo miungu watanzania ambao hata akikunyea mdomoni huna kwa kumpeleka, hapana!


Mtoto tumboni na hata mababu vitandani waheshimike katika mchakato wa kuandaa katiba mpya. Kazi ni ngumu lakini kwa kushirikiana vyema tutaiweza kwa ufanisi mkuu. Tuseme hapana kwa wale wenye nia ya kuweka taratibu fulani kwa manufaa yao, hawa ni watu wabinafi, tuwakatae kabisa!


Mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe. Jenga nchi yako kwa kuhakikisha inapata katiba mpya na imara, kuwa imara na mwenye busara katika kusimamia hilo.


Amani na upendo.

No comments:

afrotanza gallery