Tuesday, April 19, 2011

UBINAFSI

UBINAFSI umekuwa ni janga la dunia nzima, si Amerika si Ulaya si Asia, lakini kwa hapa Afrika janga hili linaonekana kushamiri zaidi kuliko sehemu zingine za dunia.

Ubinafsi, tabia ambayo imo ndani ya mtu mmoja mmoja umekuwa ni tatizo kubwa linalokwamisha maendeleo katika ngazi zote kama familia, jamii na taifa.

Ubinafsi hapa nchini umekuwa ni ugonjwa mbaya ndani ya baadhi ya watu na una athari katika nyanja muhimu katika jamii, hivyo unahitaji kupigwa vita na kila mpenda maendeleo ya nchi yetu, kwani tusipoupiga vita basi tutaendelea kuwa maskini huku wachache wakineemeka.

Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere hata kabla ya Uhuru alikuwa ameshajua kuwa Taifa lina maadui wabaya watatu, umaskini, ujinga na maradhi, hivyo aliamini Taifa haliwezi kuendelea bila kuwapiga vita maadui hao hata kama nchi itapewa uhuru wake, Hivyo baada ya uhuru alitangaza vita ya mapambano kuwatokomeza maadui hawa.

Wengi tunafahamu mafanikio ya vita hii na mojawapo hakukuwa na tofauti za kimaisha katika jamii. Naamini adui ubinafsi alikuwepo sana tu ila hakuweza kujidhihirisha waziwazi pengine kwa kumuogopa Mwalimu. Naamini pia adui huyu alifanya kazi kwa siri kubwa na kadri siku zilivyozidi kwenda aliota mizizi.

Mwalimu alipotutoka tu, adui akaanza kujidhihirisha wazi wazi,aliyekuwa amevaa mavazi ya kondoo kumbe alikuwa ni mbwa mwitu na huwezi amini hata baadhi ya watumishi na kondoo wa Mungu wamegeuka mbwa mwitu.

Watu wengi leo hii hasa wenye dhamana mbalimbali na wanaotuongoza ni wabinafsi wa kutupwa wasiojali maslahi ya walio wengi. Badala yake wanajiangalia wao na makundi yao kwanza.

La kusikitisha zaidi hata yale mawazo ya kukumbuka kuwa kuna makundi mengi ya watu katika jamii wanaohitaji mahitaji maalumu yani wasiojiweza na pia kwamba asilimia kubwa ya jamii ya watanzania inaishi katika maisha ya kifukara hawana. hata kama wanaikumbuka jamii basi ni kama vile wanasema shauri lao.

Mifano ipo mingi sana, kwa mfano maamuzi juu ya masuala yanayowagusa walio wengi sio jambo geni kusikia kiongozi fulani anaamka tu asubuhi na kutoa matamko ya maamuzi nyeti bila kuwashirikisha wataalamu na wadau mbalimbali matokeo yake maamuzi yake yanaonekana hayana tija kwa jamii.

Wasomi wetu na viongozi wetu leo hii wengi hawana habari tena ya kuitumikia jamii, wao wanaangalia maslahi yao, matumbo yao na familia zao. Mikataba mingi ya uwezekaji unakuta imesainiwa kwa kuangalia zaidi maslahi yao binafsi na sio maslahi ya jamii ya watanzania. Nani asiyejua swala la kujilimbikizia mali isivyo halali? Nani asiyejua maswala ya rushwa na ufisadi,nani asiyejua matumizi mabaya ya pesa za walipa kodi.yote haya sababu tu ya ubinafsi.

Viongozi wetu wengi leo hii wako tayari na wanaona ni haki yao kutumia pesa nyingi za walipa kodi vibaya kwa kununua magari ya kifahari ya gharama kubwa kila mwaka wakati jamii hiyo ya walipa kodi ina matatizo mengi yanayotatulika.

Inashangaza kuona hata Wabunge wetu, wawakilishi na watetezi wa wananchi Bungeni miaka ya hivi karibuni wamekuwa mstari wa mbele kudai waongezewe maslahi zaidi utafikiri hizo pesa wanakwenda kuzigawa kwenye majimbo yao. Hili limefanya hata mtu awe tayari hata kumuua mwenzie kwenye mbio za Ubunge ili yeye apite.

Katika upande wa familia, utakuta mtu ana uwezo mkubwa tu na watoto wake wanasoma hata Ulaya, lakini yeye kuwasaidia hata ada ya masomo watoto wa ndugu zake wasio na uwezo anaona shida, anaona shida hata kuwapa mtaji ndugu zake wasio na uwezo sababu ya ubinafsi, yeye anajali na kuangalia familia yake basi.

Zimwi hili la ubinafsi limekuwa likikwamisha maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi katika taifa, hivyo basi hatuna budi kulitokomeza lakini pia viongozi wa dini wasimamie hili kwani hata katika vitabu vitakatifu ubinafsi umekatazwa.

Chanzo: Mwananchi, Thursday, 17 February 2011 19:56

Amani na Upendo

No comments:

afrotanza gallery